AZAM FC imeanza vibaya kampeni yake ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Al Ahly Tripoli ya Libya.
Mchezo huo wa Kundi B uliopigwa Ijumaa, Novemba 27, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, umeshuhudia matajiri hao wa Chamazi wakishindwa kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani.
Al Ahly Tripoli ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya tisa kupitia kwa Hamdou El Houni, aliyemalizia pasi ya Muaid El Lafi.
Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Azam FC dakika ya 33 baada ya El Lafi kufunga bao la pili kwa kichwa akitumia pasi ya Mostafa Shakshak.
Hata hivyo, Zidane Sereri aliwafufulia matumaini wenyeji dakika ya 43 baada ya kufunga bao lililofanya timu hizo kwenda mapumziko huku wageni wakiongoza kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili, kikosi cha Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Florent Ibenge, kiliongeza kasi ya mashambulizi katika jitihada za kusawazisha bao hilo, lakini kilikosa umakini katika umaliziaji.
Ibenge alifanya mabadiliko kadhaa, yakiwamo ya kuwaingiza Kipre Junior na Hassan Mubiru, lakini jitihada hizo hazikuweza kubadili matokeo ya mchezo.
Licha ya Azam FC kutawala umiliki wa mpira kwa asilimia 67 na kupiga mashuti 17 dhidi ya 10 ya wapinzani wao, Al Ahly Tripoli ilifanikiwa kulinda ushindi wake hadi filimbi ya mwisho.
Mchezo huo pia ulishuhudia mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Kalala Mayele, akirejea katika ardhi ya Tanzania akiwa na kikosi cha Al Ahly Tripoli, ingawa hakufanikiwa kuziona nyavu.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuanza safari yake ya hatua ya makundi bila pointi, huku Al Ahly Tripoli ikiondoka Zanzibar na pointi tatu muhimu.
Kipigo hicho ni pigo kwa mipango ya Azam FC ya kutinga hatua ya robo fainali, ikizingatiwa kuwa kundi hilo pia linazishirikisha AS FAR ya Morocco na Durban City ya Afrika Kusini.
Azam FC sasa ina kibarua cha kujipanga upya kuelekea michezo inayofuata, huku Ibenge akihitajika kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika safu za ulinzi na ushambuliaji ili kufufua matumaini ya timu hiyo kufanya vizuri katika michuano hiyo ya kimataifa.