Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Simba SC, Murtaza Mangungu, amevunja ukimya baada ya jina lake kukosekana kwenye orodha ya awali ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti iliyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), akisisitiza kuwa bado ana nafasi ya kuendelea na safari yake ya kuwania uongozi wa klabu hiyo.
Mangungu ameeleza kuwa hatua hiyo haimaanishi mwisho wa safari yake kwa kuwa mchakato wa uchaguzi bado unaendelea. Amesisitiza kuwa atafuata taratibu zinazostahili katika hatua zinazofuata za uchaguzi.
Aidha, Mangungu amesema anashangazwa na baadhi ya watu wanaoonekana kushangilia kukosekana kwa jina lake kwenye orodha hiyo, huku akihoji madai ya kutokubalika kwake ndani ya klabu hiyo. Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu mustakabali wa uongozi wa Simba ukiendelea kugawanya maoni miongoni mwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
Katika orodha ya awali ya watu waliochukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti, Mangungu alikuwa miongoni mwa majina saba yaliyotajwa, pamoja na Anindumi Jonas Semu, Geofrey Nyange, Mohamed Soloka, Dkt. Seif Muba, Selemani Haroub Said na Swedy Mkwabi. Hata hivyo, sababu ya jina lake kukosekana kwenye orodha ya awali ya wagombea haijaelezwa.