Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amesema GSM wamedhamiria kuendelea kukiimarisha kikosi mwishoni mwa msimu ukiwa ni mpango wa muda mrefu wa kuwa na timu imara
Akizungumza na wanahabari jana baada ya mchezo dhidi ya Gwambina Fc ambao Wananchi waliondoka na ushindi wa mabao 3-1, Injinia Hersi alisema kuwa ujio wa kocha Nasredine Al Nabi ni mwanzo wa mpango huo
"Tayari tumempokea kocha wetu, leo tumekuwa nae hapa uwanjani kuishuhudia timu. Kesho (leo) ataelekea kambini Kigamboni kwa ajili ya utambulisho zaidi wa wachezaji na viongozi wengine wa benchi la ufundi. Sisi kama GSM tutaendelea kufanya maboresho yanayohitajika hatutayumbishwa na maneno ya mitandaoni"
"Umeona usajili tuliofanya umekuwa na mafanikio, mchezaji kuitwa timu ya Taifa ya DR Congo kwa mara ya kwanza akitokea klabu ya Yanga sio jambo dogo. Haya ni mafanikio makubwa. Wachezaji kama kina Yacouba, Tuisila, Bakari Mwamnyeto wamefanya mambo makubwa"
"Nataka niwahakikishie wanahabari, msimu huu ukimalizika, kuelekea msimu ujao tutafanya maboresho makubwa, tutavunja benki zinazohifadhi watu," alitamba Hersi