Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema jitihada za kutengeneza kikosi imara haziwezi kufanikiwa kama suala la nidhamu halitazingatiwa
Takribani mwezi mmoja tangu alipojiunga na Yanga, Nabi amejipambanua kwa kuwa na msimamo katika kusimamia nidhamu ya wachezaji
Kocha huyo raia wa Tunisia amesisitiza kuwa malengo hayawezi kutimia kama hakutakuwa na nidhamu. Ameeleza kuwa kila mchezaji anapaswa kuzingatia hilo na kwamba nyota waliokutana na adhabu ni mfano kwa wengine ambao wana tabia za kujiona wakubwa kuliko klabu
"Tangu nimekuja hapa nimekuwa nikifuatilia mienendo ya wachezaji wangu, nataka kujenga kikosi imara kitakachoogopeka Afrika, nitafanikiwa katika hilo iwapo suala la nidhamu litakuwa vizuri," alisema Nabi
"Nami nitasimamia hilo bila kuangalia kiwango cha mtu, anayeweza kufuata matakwa ya klabu tutaendelea kuwa naye, atakaeshindwa kuendana na kasi yetu milango iko wazi, malengo yetu ni kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa hapo mwakani"
Aidha kuhusu kikosi chake, Nabi amesema anahitaji kufanya marekebisho kadhaa ili kuendana na ukubwa wa timu kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa