Mmemsikia Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredric Mwakalebela? Amewaambia Wananchi mtakaosafiri kwenda Kigoma kushuhudia mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam kati ya Yanga dhidi ya Simba kuwa msisahau kubeba suti kwani huko kuna sherehe kubwa
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Ihefu Fc uliofuatiwa na hafla ya kumuaga kiungo Haruna Niyonzima jana, Mwakalebela alisema dhamira yao ni kuhakikish wanatwaa taji la FA baada ya kulikosa taji la VPL
"Tulipata droo nyingi hapo awali na hivyo kutupoteza kwenye malengo yetu. Lakini kwa sasa tuko vizuri, tuna kocha mzuri"
"Kwa wale watakaosafiri Kigoma waje kifua mbele na ikiwezekana waje na suti zao," alitamba Mwakalebela
Mchezo dhidi ya Simba utapigwa Julai 25 uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma
Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda ili kutawazwa mabingwa wa FA, taji ambalo wanahitaji kulipora mikononi mwa watani zao Simba
Kabla ya mchezo huo, Wananchi watakamilisha msimu wa ligi kuu mkoani Dodoma keshokutwa Jumapili kwa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji