Msimu unafikia tamati leo kwa Yanga kumaliza mchezo wa mwisho mkoani Dodoma kuwakabili watoza ushuru wa Dodoma Jiji
Yanga imemaliza msimu kwa kushika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa watetezi Simba waliotwaa ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo
Ni msimu ambao Mashabiki walikuwa na matumaini makubwa sana kwa timu yao, ni baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na GSM katika usajili
Pamoja na kwamba malengo ya kutwaa ubingwa hayakufanikiwa, lakini Wananchi watakuwa sio waungwana kama hawatathamini kile kilichofanyika
Wakati mwingine tunapaswa kukubali mafanikio hayawezi kuja mara moja, Yanga imecheza msimu huu ikiwa na wachezaji wengi wapya na makocha wanne tofauti
Tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakishindwa kuonyesha makali yao huku wengine wakichelewa kuingia mchezoni, muda ni muhimu sana katika ujenzi wa timu bora
Hata Kocha Nasreddine Nabi baada ya kusaini mkataba, aliomba sana apewe muda kuweza kujenga timu imara
Bila shaka uongozi wa Yanga hawatafanya makosa ya kukibomoa kikosi hiki kinachomaliza msimu katika nafasi ya pili
Yapo maeneo yanayohitaji maboresho ambayo kila mmoja anayafahamu lakini sio kusajili timu nzima kama ilivyokuwa misimu ya nyuma
Na sisi mashabiki turidhike, tunafurahi sana tunapoletewa wachezaji wapya tena wakati mwingine tunawaweka viongozi wetu kwenye presha kubwa tukitaka wasajili bila ya kujali mahitaji ya timu
Bahati mbaya viongozi wetu nao huwa wanauingia huu mtego na kujikuta furaha yetu ni wakati wa dirisha la usajili tu, ligi ikianza tunawakataa hata wale wachezaji tuliofurahia usajili wao na kuwakumbuka walioachwa!
Tangu ujio wa Nabi, Yanga inacheza kandanda safi na linaloeleweka, wachezaji ni hawahawa ambao baadhi yao walikuwa wakionekana dhaifu. Nabi ameweza kupata kikosi chake cha kwanza ndani ya muda mfupi
Kama kikosi hiki ataendelea nacho msimu ujao, naamini mafanikio yatapatikana makubwa
Anachohitaji ni kuongezewa watu wa kazi katika maeneo yaliyoonyesha kuwa na changamoto pamoja na kupata mbadala wa nafasi za kina Haruna Niyonzima, Carlinhos na Fiston Abdurazak
Nabi ameiongoza Yanga katika michezo 10, ameshinda michezo nane, sare moja na kupoteza mchezo mmoja
Chini yake Yanga imeshinda mechi saba mfululizo ukiwemo mchezo dhidi ya Simba uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Julai 03
Siwezi kuamini kama mtu ataniambia timu hii ni dhaifu na kuwa inahitaji maboresho makubwa
Kazi ya kocha sio kufundisha mbinu tu, pia anapaswa kutambua ubora wa wachezaji alionao na madhaifu yao pia ili kuwaimarisha pale inapowezekana
Mfano chini ya Nabi kiungo Feisal Salum amefunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao, hakufanya hivyo akiwa na makocha wengine msimu huu kwa sababu hawakufahamu eneo sahihi la kumtumia