Wakati baadhi ya wachezaji wakiondoka kujiunga na timu za Taifa kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali ya kombe la Dunia, kikosi cha Yanga kitaelekea mkoani Arusha kuweka kambi kujiandaa na mchezo dhidi ya KMC ambao utapigwa Oktoba 19
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema anaamini watakaporejea kutoka Arusha, watakuwa bora zaidi kuliko walivyo sasa
Akizungumzia mchezo dhidi ya Geita Gold ambao Yanga wameibuka na ushindi wa bao 1-0, Nabi amesema vijana wake wamecheza vizuri kulinganisha na mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar
Hata hivyo amekiri bado ipo changamoto kwenye matumizi ya nafasi, jambo ambalo ameahidi atalifanyia kazi
"Leo tulikuwa bora zaidi kulinganisha na mchezo uliopita, tulitengeneza nafasi nyingi, tumetumia nafasi moja tu. Tumecheza vizuri kwa dakika 75, kidogo kwenye dakika 15 za mwisho hatukuwa sawa, ni kawaida, hatuwezi kucheza dakika zote 90 kwa kasi ileile"
"Tunatarajia kwenda Arusha kuweka kambi, nafikiri tutakaporejea tutakuwa imara kwa muda wote wa mchezo," alisema Nabi