Katika mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc Yanga walipiga pasi zaidi ya 600, ni idadi kubwa ya pasi tena katika mchezo dhidi ya timu imara kama Azam Fc ambayo imetoka kuonyesha ubora kwenye michuano ya kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids kule Misri
Ukiwafuatilia Yanga, mchezo hadi mchezo wanaendelea kuimarika katika umiliki wa mpira
Katika mchezo huo kuna nyakati Yanga ilipiga pasi 42 pasipo kupoteza mpira huku wakifunga bao la pili baada ya kupiga pasi 22
Ni wazi sio kazi rahisi kuizuia Yanga hii yenye wachezaji mahiri katika eneo la kiungo Khalid Aucho, Yannick Bangala na Feisal Salum
Aina yao ya uchezaji ni tofauti sana, wanamiliki mpira huku wakilielekea lango la timu pinzani wakitanua uwanja na kusambaza mpira kila eneo
Yanga hii ukipaki basi utapigwa, ukifunguka utapigwa vilevile
Simba hawakupaki basi ngao ya Jamii wakapigwa, Geita Gold walipaki nasi lakini wakapigwa, Kagera Sugar, KMC na Azam Fc zote zilijaribu kufunguka nazo zikapigwa
Leo wananchi wako uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Ruvu Shooting. Msemaji wa Ruvu Shooting Massau Bwire ametamba kuwa wao ndio Barcelona ya Bongo na watakuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga
Yanga imeshazifunga timu zinazocheza mifumo tofauti, sijui Ruvu Shooting wamejipanga vipi kuweza kuepuka kipigo
Inawezekana, mpira wa miguu wakati mwingine unatoa matokeo yasiyotarajiwa lakini kwa hakika kwa hiki kikosi cha Profesa Nabi, kazi wanayo!
Morali ya wachezaji wa Yanga iko juu baada ya kushinda michezo mitano mfululizo pasipo kuruhusu bao!
Wachezaji wana ushindani wa wenyewe kwa wenyewe kuwania nafasi ya kubaki au kuingia kwenye kikosi cha kwanza
Yanga hii wanaoanza ni moto lakini pia hata ambao wako nje nao ni moto