Wananchi wameendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting
Ruvu Shooting waliziamsha hasira za Yanga baada ya kuchafua rekodi wakifunga bao kwenye dakika ya tisa kupitia kwa Shabani Msala ambaye shuti lake lilimgonga Kibwana Shomari na kumpoteza Djigui Diarra
Feisal Salum 'Fei Toto' aliirudisha Yanga mchezoni kwenye dakika ya 33 baada ya kupiga shuti kali nje ya 18, linaweza kuwa bao bora la msimu
Hilo ni bao lake la tatu msimu huu, likiwa ni bao la nne anawafunga Ruvu Shooting tangu alipojiunga na Yanga
Kipindi cha pili Yanga ilirejea kusaka mabao zaidi ya walifanikiwa kufunga bao la pili kwenye dakika ya 48 baada ya Ali Mtoni kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kuamuru mkwaju wa penati ambao uliwekwa kambani na Djuma Shabani
Mukoko Tonombe alifunga kalamu ya mabao ya Yanga kwenye dakika ya 74 akiunganisha krosi ya Farid Mussa
Ruvu Shooting watamshukuru mlinda lango wao Makaka kwani aliokoa michomo kadhaa kutoka kwa Fiston Mayele ambaye hata hivyo aliwagharimu Ruvu kumaliza pungufu
Ni ushindi wa tano mfululizo kwa Yanga katika ligi kuu ya NBC, Wananchi bado hawafungiki!


