Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema bao la dakika ya kwanza walilofungwa katika mchezo dhidi ya Biashara United lilifanya mchezo huo uonekane mgumu baada ya Wanajeshi hao wa mpakani kuwa mchezoni kwa muda mwingi
Nabi amesema walitumia muda mwingi kusaka bao la kusawazisha na baadae kuweza kupata ushindi kwenye kipindi cha pili
"Kwanza mchezo haukuwa mwepesi, nawapongeza Biashara United kwa kuonyesha mchezo mzuri. Bao walilofunga mapema liliwafanya wabaki mchezoni kwa muda mrefu. Nawapongeza wachezaji wangu walipambana kuweza kusawazisha na hatimaye kufunga bao la ushindi, hivi ndivyo timu kubwa hucheza"
"Nililazimika kubadili mfumo kwenye kipindi cha pili kwa kutumia walinzi watatu nyuma, mabadiliko hayo yalitusaidia tukapata bao lakini baadae tukalazimika kurejea katika mfumo wa walinzi wanne baada ya Biashara United kuja juu kusaka bao la kusawazisha," alisema Nabi
Biashara United ilitangulia kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya kwanza kupitia kwa Atupele Green aliyemalizia mpira uliokuwa umetemwa na mlinda lango Djigui Diarra
Yanga ilisawazisha bao hilo kwenye dakika ya 40 kupitia tik-tak ya Fiston Mayele
Katika dakika ya 79 Jesus Moloko akafanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na Abdulmajid Mangalu na mwamuzi kuizawadia Yanga mkwaju wa penati uliowekwa kimiani na Saido Ntibazonkiza
Ni ushindi ambao umeifanya Yanga ijichimbie kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tano baada ya kufikisha alama 26