Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wako tayari kwa mchezo wa pili wa kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM ambao utapigwa saa kumi jioni kwenye uwanja wa Amaan.
Kaze amepewa jukumu la kukiongoza kikosi cha Yanga kwenye michuano hiyo ambayo alishinda mwaka 2021
Kocha huyo raia wa Burundi amesema anaifahamu vyema KMKM kwakuwa wamecheza nayo kipindi cha miezi miwili iliyopita hivyo amejiandaa vyema na kikosi chake kuelekea mchezo huo.
"Ni timu nzuri yenye vijana wenye uwezo mzuri wa kukaa na mpira, kushambulia na kukaba kwa umakini mkubwa hivyo tumefanyia mazoezi mbinu mbalimbali kuhakikisha tunakuwa bora juu yao," alisema Kaze
Kaze amesema kwa sasa Yanga imekamilika hivyo ana imani kubwa wachezaji watakaopewa nafasi kwenye mchezo huo watafanya vizuri
"Kwa sasa tuna kikosi kipana chenye wachezaji wengi wazuri . Daima nawaelezea, mwenye jitihada na uwezo wa kufuata maagizo ambayo tunawapa mazoezini, atapata kipaumbele cha kuitumikia klabu. Uzuri wachezaji wote wana nidhamu nzuri ya uwanjani na maisha binafsi"
Yanga leo wanacheza mchezo wao wa pili katika michuano ya Mapinduzi milango ya saa 10:15 jioni. Mchezo wa kwanza walicheza na Taifa Jang'ombe na kushinda goli 2-0 . Magoli hayo yalitiwa kambani na Heritier Makambo na kinda Denis Nkane usajili mpya wa dirisha dogo kutoka Biashara United