Wananchi 'wameteka shoo' huko mkoani Tanga wakipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Mkwakwani
Ulikuwa ushindi wa kibabe kwa Yanga ambayo imemaliza umwamba wa miaka saba wa Coastal Union dhidi ya Yanga katika uwanja wa Mkwakwani
Itoshe kusema Wananchi wanaonyesha kwa vitendo kuwa wanautaka ubingwa wa ligi kuu ya NBC msimu huu
Fiston Kalala Mayele ameendeleza umahiri wake katika kuzifumania nyavu akifunga bao la kuongoza kwenye dakika ya 42 akimalizia krosi ya Juma Shabani

Yanga ingeenda mapumziko ikiwa na mabao zaidi ya matatu kama Saido na Jesus Moloko wangetumia nafasi walizopata
Coastal Union walicheza mchezo wa nguvu zaidi huku Yanga ikijitahidi kuweka mpira chini licha ya changamoto ya uwanja wa Mkwakwani
Mabadiliko ya kuingia Farid Mussa na Dickson Ambundo nafasi za Feisal Salum na Jesus Moloko na baadae Heritier Makambo kuingia nafasi ya Mayele, yaliinufaisha Yanga kwani Farid alitengeneza bao la pili lililowekwa kambani na Saido kwenye dakika za majeruhi
Ni ushindi wa heshima kwa Yanga mkoani Tanga. Kulikuwa na ahadi lukuki za fedha (zaidi ya Mil 50) kwa Coastal Union kama wangepata ushindi dhidi ya Yanga
Lakini wameangukiwa na kitu kizito. Mwananchi huyoooo ameondoka na alama tatu