Uongozi wa klabu ya Yanga umeitaka Bodi ya Ligi kutimiza wajibu wake kuhakikisha wanalinda hadhi ya ligi kuu isichafuliwe na watu wachache
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari leo, Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema hawaridhishwi na mwenendo wa uendeshaji wa ligi hasa kutokana na matukio ya upendeleo kutoka kwa waamuzi
Bumbuli ametoa takwimu zinazoonyesha ni kwa kiasi gani Simba imekuwa ikinufaika na makosa ya waamuzi katika michezo tisa
"Tunaongoza Ligi hii kwa tofauti ya alama tano (5), tukiwa na matumaini makubwa sana ya kwamba tuna kikosi imara na tunakwenda kushinda ubingwa msimu huu"
"Pamoja na hayo yote Klabu ya Yanga tunapenda kueleza kwamba haturidhishwi na mwenendo wa baadhi waamuzi wanaocheza michezo ya Ligi kuu"
"Hii imetokana na mlolongo wa matukio ya maamuzi yenye utata ambayo Kwa namna moja au nyingine yananyima haki ya timu zingine na yanatoa manufaa Kwa timu zingine"
"Yanga wamecheza mechi 14 dakika zilizoongezwa ni 34, kwenye michezo 15 ya Simba walizocheza wameongezewa dk 75, Simba wanaongezewa dk 7 dk 9 nk lakini Yanga dakika 2,3,4 pia Simba ndio timu inayoongoza kwa Penati," alisema Bumbuli
Bumbuli amesema Yanga kama taasisi hawaombi wapendelewe lakini wanachotaka ni kuona ligi inaendeshwa kwa usawa kwa timu zote na sio timu moja kuonekana inanufaika zaidi katika matukio yenye utata