Wakati kikosi cha Yanga kikitua salama jijini Mwanza, mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo, Fiston Mayele ameweka wazi anapambana kuhakikisha anaibuka na tuzo ya ufungaji bora lakini pia akilenga kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu
Yanga imetua Mwanza kwa ajili ya mechi yake dhidi ya wenyeji Geita Gold FC kutoka mkoani Geita kuuchagua Uwanja wa CCM Kirumba kutumika hapo kesho.
Mayele ameshafunga mabao tisa akiwa nyuma ya mshambuliaji wa Namungo FC, Reliants Lusajo ambaye ametikisa nyavu za wapinzani mara 10.
Mayele amesema kuwa malengo yake makubwa ni kuona Yanga inapata matokeo mazuri katika kila mechi huku akiongeza umakini wa kutumia nafasi za kufunga mabao anazopata.
"Ligi imekuwa na ushindani mkubwa, nitapambana kutimiza malengo yangu kuhakikisha natumia vizuri nafasi tunazopata kuendelea kufunga mabao na timu yangu kufikia malengo yetu," alisema Mayele.
Mkongomani huyo alisema wakati akihitaji kuchukua tuzo ya ufungaji bora angependa kuona wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanaendelea kufurahi.
"Kila mechi ni ngumu na kila timu imejipanga kutafuta matokeo mazuri hasa kipindi hiki cha mechi za duru la pili, kwetu tunahitaji kuendelea kutafuta pointi muhimu ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi," alisema Mayele.
Aliongeza hana presha na kiwango chake cha kufumania nyavu na anachongalia zaidi ni kupambana katika kila mechi ili wapate kile wanachokitarajia