Leo majira ya saa moja usiku Yanga itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Namungo Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Wananchi wanakabiliwa na mtihani mwingine ambao kama watafanikiwa kuvuka basi watazidi kukaribia ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Nje ya uwanja kumekuwa na tambo nyingi hasa kutoka kwa Namungo Fc ambao kocha wao Msaidizi Jamhuri Kiwhelo 'Julio' ametamba watakuwa timu ya kwanza kupata ushindi dhidi ya Yanga msimu huu
Matokeo ya mchezo wa kwanza uliopigwa kule Lindi na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 ndio yanayowapa jeuri Namungo kuona wanaweza kuisimamisha Yanga katika dimba la Mkapa
Aidha mchezo wa leo ni wa sita kwa Yanga na Namungo Fc kukutana kwenye ligi, hakuna timu iliyopata ushindi katika michezo mitano iliyopita
Namungo Fc leo watapata mashabiki wengi kutoka kwa wapinzani wa Yanga (Simba) ambao wanaamini kama Yanga itapoteza mchezo wa leo, watarejesha matumaini katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu
Kauli zilizotolewa na kocha msaidizi wa Namungo Fc jana, ni kama zimedokeza jambo kuwa Namungo wameandaliwa kwelikweli kuhakikisha wanaisimamisha Yanga leo
Hata hivyo ni wazi itakuwa vita ngumu kwao kupigana na Yanga hasa inapokuwa kwenye ubora wake
Msimu huu Yanga imeshinda michezo migumu zaidi ya mchezo wa leo tena katika mazingira ambayo wengi waliamini Yanga haiwezi kupata matokeo
Namungo wanakwenda kukutana na timu ambayo imeshinda mechi 16 na kutoka sare michezo mitatu tu kwenye ligi, ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na alama 51
Wananchi wako mbele ya Namungo Fc kwa alama 22, ukubwa huu wa tofauti ya alama unaakisi tofauti ya ubora kati ya timu hizo mbili
Wanakwenda kukutana na Yanga ambayo itakuwa na wachezaji wake wote muhimu ambao michezo ya karibuni walikosekana kutokana na majeraha
Jesus Moloko, Feisal Salum, Khalid Aucho, Chico Ushindi, Farid Mussa wote wamerejea na wanaweza kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga leo
Saido Ntibazonkiza na Yacouba Songne ndio wachezaji ambao watakosekana kutokana na majeraha
Kwa Yanga huu ni mchezo ambao wanazihitaji alama zote tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu
Ushindi utafungua tofauti ya alama dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili kuwa 13 matokeo ambayo yatawaweka nafasi nzuri kisaikolojia kuelekea mchezo dhidi ya Simba April 30