Wananchi hawapoi! ndivyo unavyoweza kusema kwani licha ya kuwa tayari wametwaa ubingwa wa ligi kuu, Yanga imeendelea kutembeza dozi baada ya leo kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilitosha kuihakikishia Yanga ushindi muhimu kwa mabao ya Feisal Salum dakika ya 12 akiachia kombora la mguu wa kushoto baada ya pasi ya Fiston Mayele na Chico Ushindi akafunga bao la pili dakika ya 17 kwa shuti kali kutoka nje ya 18
Yanga iliendelea kutawala mchezo huo kwenye kipindi cha pili lakini hawakufanikiwa kuongeza mabao licha ya kutengeneza nafasi kadhaa
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi leo alifanya mabadiliko kidogo kwenye kikosi chake akimuanzisha mlinzi Ibrahim Bacca ambaye alionyesha kiwango bora
Mshambuliaji Chico Ushindi ameendelea kuwafunga midomo wakosoaji wake kwani amefunga katika mchezo wa pili mfululizo
Yanga imefikisha alama 70 na kuendelea kujitenga zaidi katika msimamo wa ligi huku wakiwa tayari ni mabingwa
Aidha Polisi Tanzania waliipa Yanga heshima ya kuwa mabingwa kwa kuwawekea 'guard of honor' wakati wakiingia uwanjani



