Winga machachari wa Yanga, Bernard Morrison baada ya kukosekana katika michezo miwili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini, amesema yupo fiti kurejea uwanjani kuisaidia timu yake katika michuano hiyo ya hatua inayofuata dhidi ya Al Hilal ya Sudan
Morrison hakuonekana katika michezo hiyo miwili kutokana na kusumbuliwa na majeraha, lakini Yanga ilifanikiwa kutinga raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0, ikishinda 4-0 mechi ya kwanza na 5-0 ya marudiano.
Nyota huyo raia wa Ghana asiyeishiwa vituko, amesema amepona na atarejea uwanjani hivi karibuni, hivyo kwa kushirikiana na wenzake atahakikisha anapambana kuisaidia timu yao kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa hadi kufikia malengo yao.
Amesema malengo yao makubwa ni kuona Yanga inacheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na anaimani hilo litafanikiwa kwa sababu ya ubora wa kikosi cha timu yao.
"Ni kweli sijaonekana uwanjani kwa sababu ya majeruhi na sasa niko vizuri, nimeanza mazoezi na nitarudi uwanjani kupambania timu kupata matokeo mazuri katika michezo iliyopo mbele yetu," alisema Morrison
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa atatumia michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu Fc na Ruvu Shooting kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal watakaoanzia nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 8, mwaka huu.
Kikosi cha Yanga kimeanza mazoezi leo kujiandaa na michezo iliyo mbele yao