Mkurugenzi wa Maendeleo ya soka la Vijana Yanga, Mwinyi Zahera amesema wana kikosi imara chenye uwezo wa kupata ushindi dhidi ya Al Hilal hata hivyo ni jukumu la wachezaji kupambana kuhakikisha wanafanikisha hilo
Zahera atakuwa msaada mkubwa kwa Kocha Nasreddine Nabi kuelekea mchezo huo kwani kwa muda mrefu amefanya kazi kwa karibu na Florent Ibenge katika timu ya Taifa ya DR Congo akiwa kocha msaidizi
Amesema kazi ya benchi la ufundi ni kuwasoma Al Hilal na kuandaa mbinu za kuwakabili uwanjani, jukumu litakalobaki ni wachezaji wenyewe kutambua kazi iliyopo mbele yao
"Kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza anatakiwa kujiamini na kutumiza majukumu yake yalivyo, kila mchezaji anatakiwa kupandisha ubora wake zaidi ya kawaida"
"Ni lazima wachezaji wajitolee kwa asilimia mia ikitokea wakacheza kwa asilimia 70, maana yake hawataweza kushindana na wenzao kwani watakuja na ubora kuliko wao," Zahera alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Mcongomani huyo amesema Yanga ina faida zaidi dhidi ya Al Hilal kwa kuwa tayari ina wachezaji wenye uzoefu wa kushiriki michuano mikubwa. Ufanisi wa wachezaji hao katika mchezo huo ni muhimu sana kwa Yanga
Lakini pia amesema Yanga ina wachezaji wengi waliowahi kufanya kazi na Ibenge hivyo kwa namna moja inaweza kuwa faida kwao kwani wanafahamu vyema mbinu zake
Kocha Nabi nae amewahi kuzifundisha Al Hilal na El Mareikh timu hasimu katika ligi kuu ya Sudan hivyo anafahamu vyema aina ya mchezo ambao timu yake inakwenda kukabiliana nao