Timu ya Al Hilal ya Sudan imewasili nchini wakitokea DR Congo walikoweka kambi ya muda mfupi
Al Hilal watakuwa wageni wa Yanga siku ya Jumamosi kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi
Akizungumza na wanahabari baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, kocha wa timu hiyo Florente Ibenge amesema wanatarajia mchezo wenye ushindani kutoka kwa Yanga
Ibenge amesema anafahamu Yanga ina wachezaji wengi wazuri akiwemo mshambuliaji Fiston Mayele aliye katika kiwango bora
"Huu ni wakati wa Mayele yuko katika kiwango bora sana lakini hatutaangalia mchezaji mmoja kwani tunafahamu Yanga ina wachezaji wengi wazuri hivyo najua utakuwa mchezo mgumu," alisema Ibenge
Ibenge pia aliwataja Jesus Moloko, Yannick Bangala, Juma Shaban, Joyce Lomalisa, Tuisila Kisinda na Bernard Morrison kuwa wachezaji aliowahi kufanya nao kazi na atakutana nao wakiwa na Yanga siku ya Jumamosi