Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema wanaheshimu maoni ya wachambuzi wa soka nchini kwani dhamira ya Yanga ni kushirikiana na vyombo vyote vya habari
Baada ya Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa mkondo wa kwanza ligi ya mabingwa barani Afrika, wapo wachambuzi ambao wamejigeuza waganga na watabiri ambao wanaamini Yanga haina ubavu wa kuifunga Al Hilal huko Sudan
Kamwe amesema wanaheshimu maoni yao kama wanavyoheshimu maoni ya wale wanaoamini hakuna jambo lisilowezekana kwenye mpira wa miguu
"Hatupo hapa kumzuia mchambuzi yeyote kuizungumzia Yanga, tupo hapa kushirikiana na vyombo vya habari na wachambuzi kuhakikisha Yanga inakuwa brand kubwa Afrika"
"Kila mchambuzi ambaye anafanya kazi kwenye chombo cha habari anaaminika, hayupo kwa bahati mbaya. Yanga hatuwezi kuingilia maoni yake, maoni yanatolewa sehemu yoyote duniani"
"Kama wanaamini Yanga hawezi kufanya vizuri Khartoum, tunaheshimu maoni yao, sisi tunaamini kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Hatuwezi kujibizana nao, kazi yetu ni kucheza mpira"
"Wanaosema timu yetu haiwezi kufuzu, tukifuzu watakuwa upande wetu na wataelezea kitaalam kwa nini tumefuzu. Kwa hiyo tunaheshimu mawazo yao na tunaomba waendelee kuizungumza timu yetu ili tupate mahali pa kuboresha kutoka kwenye maoni wanayotoa," alisema Kamwe
Yanga itaondoka nchini Alfajiri ya kuamkia kesho Jumamosi kuelekea Sudan tayari kwa mchezo dhidi ya Al Hilal ambao utapigwa Jumapili usiku (saa 3)