Baada ya kukosekana katika mechi tatu zilizopita akitumikia adhabu, kiungo fundi wa mpira Stephane Aziz Ki leo atakuwa dimbani kuwakabili Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Aziz Ki alishiriki kikamilifu mazoezi ya mwisho Yanga jana Avic Town tayari kwa mchezo huo muhimu
Wananchi leo watamkosa kiungo mwingine fundi Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano
Hata hivyo upana wa kikosi cha Yanga utaendelea kudhihiri kwani kila nafasi imesheheni wachezaji mafundi kwelikweli
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi huenda leo akawatumia Khalid Aucho na Salum Abubakar 'Sure Boy' katika eneo la kiungo huku Aziz Ki akicheza namba 10 sambamba na Fiston Mayele
Kiraka Yannick Bangala leo anatarajiwa kurejea kikosini na pengine anaweza kutumika katika safu ya ulinzi sambamba na Dickson Job
Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto licha ya kurejea kikosini alipata changamoto kwenye mchezo uliopita, pengine Nabi hatahitaji kuharakisha kumrejesha kikosini
Joyce Lomalisa kwa sasa amejihakikishia nafasi safu ya ulinzi upande wa kushoto kama ilivyo kwa Kibwana Shomari ambaye sasa anampa wakati mgumu Djuma Shaban upande wa kulia
Hata hivyo, Djuma amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara
Mlinda lango namba moja Djigui Diarra amerejea kama ilivyo kwa Bernard Morrison ambaye alikosa mchezo uliopita kutokana na matatizo ya kifamilia
Katika mtanange wa leo Yanga itaingia na shauku ya kushinda na kuendeleza rekodi yao ya 'unbeaten' na muhimu zaidi kuendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi