Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema lengo la klabu hiyo ni kutetea mataji waliyoshinda msimu uliopita, unbeaten ilikuwa sehemu ya mafanikio waliyopata katika kukamilisha malengo yao
Juzi Yanga ilipoteza mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Ihefu Fc wakifungwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Highland Estates, Mbeya
Ni matokeo ambayo yameibua shangwe kwa wapinzani wao ambao wamekuwa katika sherehe kubwa kwa siku mbili zilizopita
Kamwe amesema 'unbeaten' ya mechi 49 ni rekodi ambayo wameiweka katika mchakato wao wa kusaka ubingwa lakini hawakuwa wakicheza kwa ajili ya 'unbeaten' kwani hakuna ubingwa wa 'unbeaten'
Aidha, Kamwe ameeleza kushangazwa na dhihaka inayofanyiwa Yanga baada ya kupoteza mchezo, na haoni pongezi kwa Ihefu Fc kwa kufanikiwa kuizuia Yanga
"Nashangazwa na dhihaka kuwa kubwa zaidi kwa Yanga kuliko pongezi ambazo wanapaswa kupewa Ihefu Fc. Sio jambo dogo kwao kupata ushindi dhidi yetu baada ya timu nyingine 49 kushindwa lakini kinachoonekana ni Yanga kudhihakiwa zaidi kuliko Ihefu Fc kutambuliwa kwa mafanikio waliyopata"
"Kule Uingereza, Manchester United inatajwa na zaidi unapozungumzia unbeaten ya mechi 49 iliyowekwa na Arsenal. Ni kwa sababu wao ndio waliosimamisha rekodi hiyo," alisema Kamwe
Katika hatua nyingine, Kamwe amesema Yanga imerejea mazoezini kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Jumapili, Disemba 04 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 1 usiku
Kamwe amesema wanatambua umuhimu na ugumu wa mchezo huu lakini wachezaji wao wako tayari kusaka alama tatu
"Tunatambua Prisons ni timu ngumu kutokana na aina ya mbinu ambazo hutumia hasa wanapokutana na hizi timu kubwa. Jambo jema kwetu ni kuwa wachezaji wetu wako tayari wamesahau matokeo ya mchezo uliopita. Wanajua hii ni nafasi kwao kuwapa furaha mashabiki wao baada ya kupoteza mchezo uliopita"
Silent Ocean ambao ni Wadhamini wa Tanzania Prisons wameahidi kutoa Tsh Milioni 20 kwa timu hiyo kama itapata ushindi dhidi ya Yanga na Tsh Milioni 10 kama watapata sare