Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji Said Sudi amesema wamejiridhisha pasipo na shaka kuwa Feisal Salum ana mkataba halali na klabu ya Yanga
Sudi amesema kamati yao imelifunga shauri hilo lakini kama Feisal hakuridhishwa na maamuzi ya kamati, atapewa 'review' aende Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS)
"Feisal ni Mchezaji halali wa Yanga na tumepitia mkataba unaonesha wazi ni mali yao, ila kama hajaridhika na maamuzi yetu anayo nafasi ya kukata rufaa na sisi tutampa review aende CAS sio hapa tena," alisema Sudi akihojiwa kwenye kipindi cha michezo TBC Taifa
Baada ya maamuzi hayo ya Kamati, Feisal anapaswa kurejea kambini Avic Town kuendelea na majukumu yake katika kikosi cha Yanga
Kama hataripoti ina maana atakuwa anaendelea kuvunja makubaliano ya kimkataba jambo ambalo linaweza kumuweka matatani zaidi kwani kama Yanga itaamua kumchukulia hatua anaweza kufungiwa kucheza soka kwa muda mrefu
Ni wazi Yanga iko tayari kuachana na Feisal lakini wanachotaka ni mchezaji huyo kufuata taratibu kama zilivyoainishwa katika mkataba wake
Klabu ambayo inataka kumsajili Feisal inapaswa kukaa mezani na Yanga ili kukubaliana dau la usajili la mchezaji huyo kwa kuzingatia thamani yake ya sasa
Feisal alisaini mkataba wenye thamani ya Tsh Milioni 100 mwaka 2020, ni wazi thamani yake ya sasa sio sawa na ile aliyokuwa nayo mwaka 2020
Njia rahisi kwa Feisal kuondoka Yanga kabla ya mkataba wake kumalizika ni kwa hiyo timu inayomtaka kufika meza ya majadiliano na Yanga
Tetesi zinaihusisha Azam Fc na Feisal, uamuzi ni wao, kama wanamtaka kweli Feisal basi wakamilishe mchakato wa usajili wake kwa kufuata taratibu
Kutumia njia za mkato wakati mwingine ni hatari na zaidi atakayeumia zaidi ni Feisal ambaye anaweza kupoteza kipaji chake