Kiungo wa Yanga Khalid Aucho amesema kushinda mataji ndio jambo muhimu kwake kuliko tuzo binafsi
Licha ya kuwa na msimu mzuri kwenye ligi, Aucho sio miongoni mwa wachezaji waliotajwa na TFF kuwania tuzo mbalimbali msimu huu
Kukosekana kwake kuliibua mijadala mikali miongoni mwa wadau wakihoji imekuwaje fundi huyu hajaonekana katika tuzo?
Hata hivyo Aucho amesema hilo sio jambo muhimu sana kwake zaidi ya kuisaidia Yanga kushinda mataji
"Tuzo sio kipaumbele huu ni muda wetu sisi kama wachezaji kuzingatia michezo miwili migumu iliyo mbele yetu kuhakikisha tunatwaa taji la Afrika kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo imeanzishwa tukiwa ndani ya timu hii"
"Nikichukua tuzo ni ya kwangu binafsi timu hakuna inachokiingiza lakini nikiwa miongoni mwa wachezaji watakaoifanya Yanga inatwaa taji la Afrika ni rekodi kubwa itaandikwa vizazi hadi vizazi"
"Kila mchezaji ana malengo yake mimi napenda kuwa mchezaji ambaye anaipa timu yake mafanikio kama kutwaa mataji, kufika hatua kubwa kwenye mashindano hilo nimeweza kulifanikisha kwa misimu miwili niliyocheza Yanga." alisema Aucho
Katika msimu huu Aucho amekuwa 'injini' ya kikosi cha kocha Nasreddine Nabi akiwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi
Hata hivyo atakosa mchezo wa mkondo wa kwanza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger ambao utapigwa Jumapili, May 28 katika uwanja wa Benjamin Mkapa