Msimu wa ligi kuu 2022/23 umefikia tamati kwa Yanga kubeba mataji yote ya ndani ukiwa ni msimu wa pili mfululizo Wananchi 'kusepa' na kila taji
Baada ya kusherehekea mafanikio makubwa msimu huu, uongozi wa Yanga una kazi ya kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi lililoipa Yanga mafanikio hayo linaendelea kubaki
Msimu uliomalizika Yanga imecheza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika, mikakati iliyowekwa kwa msimu ujao, ni Yanga kucheza hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, haya ni malengo ya chini kabisa
Jukumu la kwanza la Mtendaji Mkuu Andre Mtine ni kuhakikisha anambakisha Kocha Mkuu Nasredine Nabi na Msaidizi Cedric Kaze pamoja na mshambuliaji Fiston Mayele
Mikataba ya Nabi na Kaze imemalizika, mazungumzo ya kuhuisha mikataba yanaendelea. Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amewahakikishia Wananchi kuwa watafanya kila jitihada kuhakikisha Nabi anaendelea kubaki Jangwani
Ni wazi, Nabi amelijenga jina lake baada ya kuipeleka Yanga fainali ya kombe la Shirikisho, mwenyewe amethibitisha zipo ofa mezani lakini bado anaipa kipaumbele Yanga
Mayele bado ana mkataba na Yanga lakini ofa zimeendelea kumiminika Jangwani kumtaka mfungaji huyo bora wa ligi na michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Ili kumbakisha Yanga inalazimika kuboresha maslahi yake zaidi, jambo ambalo Injinia Hersi ameahidi watalifanya