Ligi Kuu imeanza kwa kishindo, licha ya Yanga kutoshuka dimbani, mpaka sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi
Jana lilitokea tukio la aina yake kwa klabu ya Kitayosce Fc kuchuana na Azam Fc ikiwa na wachezaji nane uwanjani baada ya wachezaji wengine kuzuiliwa kwa kilichoelezwa kuwa hawakuwa na sifa za kucheza ligi kuu msimu huu
Ulikuwa mchezo ambao Kitayosce wangeweza kufungwa idadi yoyote ya mabao kama sio wachezaji wake wawili kuumia na hivyo mchezo huo kutoendelea kwa kuzingatia kanuni inayoelekeza kila timu lazima iwe na wachezaji wasiopungua saba uwanjani
Baadhi ya wadau wamehoji kulikuwa na ulazima wa mchezo huo kuchezwa jana kutokana na kile kilichoikumba Kitayosce (Tabora United), ambayo ilifungiwa kusajili na FIFA na baadae hukumu hiyo kubatilishwa baada ya kumalizana na wachezaji waliokuwa wakiidai timu hiyo
Msimu uliopita kuna timu mechi zake ziliahirishwa kwa sababu walichelewa kurudi pre-season kutoka Dubai
Yaani timu ilienda pre-season wakati ligi inaendelea na walipochelewa mechi zao zikasogezwa mbele
Pia haijasahaulika timu hiyohiyo msimu mmoja nyuma, mechi yake dhidi ya Kagera Sugar iliahirishwa kwa sababu wachezaji wake 16 walikuwa wagonjwa!
Na taarifa ikaeleza kuwa timu hiyo imebaki na wachezaji saba, hivyo mechi yake ikaahirishwa. Lakini jana Kitayosce waliambiwa lazima waingie uwanjani kwa sababu idadi yao inakidhi vigezo. Kama Kitayosce waliomba mechi hiyo iahirishwe ilipaswa busara itumike tu kama ilivyotumika kwa wengine huko nyuma
Jana kulikuwa na uwezekano mkubwa mfungaji bora wa ligi kuu ya NBC 2023/24 angepatikana!
Maana ni wazi wachezaji wa Azam Fc wangeshindana kufunga mabao kadiri wanavyoweza kwani hawakuwa na upinzani kutoka kwa wapinzani wao waliokuwa saba uwanjani na golikipa wa nane
Thamani ya ligi yetu tunapaswa kuilinda kwa kutoruhusu aibu na fedheha ndogondogo. Pata picha wale Kitayosce wangefungwa mabao 30 na bado tungetamba ligi yetu ni bora?