Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amewapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya ushindi wa jumla wa mabao 3-0 dhidi ya Al Merrikh
Akizungumza baada ya mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa uwanja wa Azam Complex na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, Gamondi alisema walistahili kutinga hatua ya makundi ambayo hawakushiriki kwa takribani miaka 25
"Nawapongeza wachezaji kwa ushindi wa leo, tulitawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi. Tuliwadhibiti vyema wapinzani wetu kwani hawakutengeneza nafasi yoyote ya hatari"
"Wakati mwingine sio rahisi kucheza mechi muhimu mbele ya mashabiki wako ukicheza dhidi ya timu ambayo haina cha kupoteza lakini nafurahi tumeweza kuibuka na ushindi"
"Nampongeza Rais wa klabu (Injinia Hersi), uongozi wote, wenzangu benchi la ufundi na wachezaji kwa kufanikisha malengo yetu na kuwapa furaha Wananchi ambao wamesubiri kwa miaka 25 kucheza hatua ya makundi. Kwa hakika tumestahili kufikia mafanikio haya," alisema Gamondi
Akichukua majukumu yaliyoachwa na Nasreddine Nabi, kocha Gamondi ameweza kuifanya Yanga kuwa bora zaidi licha ya maingizo ya wachezaji kadhaa wapya na kufanikiwa kuipeleka hatua ya makundi CAF CL
Nabi aliyetimkia FAR Rabat kwa upande wake mambo hayakuwa mazuri kwani ameshindwa kuisaidia timu hiyo kutinga makundi baada ya kufungwa mabao 2-1 nyumbani na Etoile Du Sahel
FAR Rabat waliondoshwa kwa kufungwa jumla ya mabao 3-1 na Etoile kutoka Tunisia