Baada ya mapumziko ya takribani siku 16, Yanga inarejea leo kwenye mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC ambao majira ya saa 12:30 jioni watakuwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Azam Fc katika mwendelezo wa ligi mzunguuko wa sita
Alama tatu za mchezo huu zina umuhimu mkubwa kwa Yanga kwani ni matokeo ambayo yatawashuhudia Wananchi wakirudi kileleni mwa msimamo wa ligi
Timu hizo zimetenganishwa na alama moja tu katika msimamo wa ligi Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 12 wakati Azam Fc wako nafasi ya pili wakiwa na alama 13
Ni wazi hautakuwa mchezo mwepesi, hii ni Dar es salaam derby, mechi inayokuwa na ushindani zaidi ukitoa mchezo wa watani wa jadi
Yanga imekuwa na takwimu nzuri dhidi ya Azam Fc katika misimu ya karibuni kwani katika mechi sita zilizokutanisha timu hizo katika mashindano yote, Yanga imeshinda mechi tano huku mchezo mmoja ukimalizika kwa sare
Ukiangalia aina ya usajili ambao Azam Fc walifanya katika dirisha lililopita kwa kusajili waliokuwa wachezaji wa Yanga, ni wazi inaonyesha ni kwa kiasi gani vipigo dhidi ya Yanga vinawatesa wakiamini kusajili baadhi ya wachezaji kungeipunguzia nguvu Yanga
Feisal Salum, Yannick Bangala na Djuma Shaban wote walisajiliwa na Azam Fc wakitokea Yanga
Hata hivyo Djuma alichelewa kuandikishwa kwenye mfumo wa usajili na hivyo ataanza kuitumikia timu hiyo baada ya dirisha dogo kufunguliwa
Ni wazi bado haitakuwa rahisi kwa Azam Fc kuondoka na alama tatu dhidi ya Yanga kutokana na ubora wa kikosi cha kocha Miguel Gamondi
Msimu huu Yanga imejipambanua kwa kucheza soka la kasi huku ikifunga mabao kutoka kila upande
Gamondi anafahamu hahitaji kupoteza mchezo mwingine baada ya kipigo cha Ihefu Fc kwani matokeo tofauti na ushindi yanaweza kuwaongezea matumaini watani zao Simba katika mbio za ubingwa
Wanasema biashara ni asubuhi, huu ndio wakati mzuri wa Yanga kuvuna alama katika mechi muhimu ili kujipalilia njia ya kutetea ubingwa msimu wa tatu mfululizo
Kama Yanga itashinda mechi tatu zinazofuata kuanzia mchezo dhidi ya Azam Fc leo, ni wazi itakuwa imejiweka katika mazingira mazuri
Baada ya Azam Fc mechi zitakazofuata ni dhidi ya Singida BS na Simba