Dakika 20 alizocheza katika mchezo dhidi ya Singida BS zilionyesha utayari wa winga fundi Skudu Mabudubela na pengine anaweza kuwa sehemu ya wachezaji watakaoikabili Simba siku ya Jumapili
Uwezo wake wa kuwavuruga mabeki inaweza kuwa silaha muhimu kwa Yanga katika mchezo huo hasa kama ataingia katika muda ambao presha ya mchezo itakuwa imepungua
Aina yake ya uchezaji inamfanya Skudu kukamiwa na walinzi wa timu pinzani lakini pia presha nyingine inatokana na vile Yanga ilivyopamba usajili wake
Nyota huyo aliyeng'ara na kikosi cha Marumo Gallants msimu uliopita, anafahamu bado ana deni kubwa kwa Wananchi
Ameendelea kuzoea mazingira na ligi kuu ya Tanzania Bara huku Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi akimtumia kwa tahadharia kuhakikisha hamuweki kwenye presha kubwa
Katika moja ya mahojiano yake Skudu alisema anafurahi kucheza Yanga, ataendelea kupambana kila anapopewa nafasi ili kuhakikisha anachangia kutimiza malengo ya timu ambayo ni kushinda kila mchezo