Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga wako nchini Algeria kuipeperusha bendera ya Tanzania katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika
Wananchi watakuwa wageni ya CR Belouizdad katika mchezo utakaopigwa saa 4 usiku kwa saa za Tanzania ambapo huko Algeria itakuwa saa 2 usiku
Yanga imeweka malengo ya angalau kuvuka hatua hii ya makundi kwenda robo fainali, watahitaji kuanza kukusanya alama ugenini ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo
Yanga ina rekodi ya aina yake katika mechi za ugenini kwenye michuano ya CAF ikishinda mechi sita mfululizo walizocheza ugenini
Ni nafasi nyingine kwa Yanga inayonolewa na kocha Miguel Gamondi kuendeleza rekodi ya ubabe katika mechi za ugenini Kimataifa
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Algeria, CR Belouizdad ambao wanaaminika kuwa timu bora zaidi hapo Algeria
Belouizdad ni miongoni mwa timu ambazo zilitangazwa na CAF kuwania tuzo ya klabu bora ya mwaka kama ilivyo Yanga lakini wao wameshindwa kupenya katika mchujo wa pili uliobakisha timu tano Yanga ikiwemo
Mchezo utapigwa uwanja wa July 05, Yanga ina kumbukumbu na uwanja huu kwani msimu uliopita walishinda bao 1-0 dhidi ya USM Alger kwenye mchezo wa pili wa fainali CAF CC katika mchezo ambao uligubikwa na matukio mengi ya nje ya uwanja
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wanatambua ugumu wa mchezo huo lakini watakwenda kucheza soka lao huku wakiwaheshimu wapinzani wao
Wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo, Gamondi atakuwa na uhakika wa kuwatumia wachezaji wake bora watakaowapa Wananchi furaha