Bao la dakika ya 97 lililofungwa na Nickson Kibabage limeihakikishia Yanga alama tatu muhimu dhidi ya Jamus Fc baada ya ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa kombe la Mapinduzi uliopigwa uwanja wa New Amaan Complex
Haikuwa mechi rahisi, wachezaji wa Yanga walihitaji uvumilivu na utulivu kuweza kupata ushindi mbele ya Jamus Fc waliokuwa na nidhamu kubwa katika kujilinda
Farid Mussa aliitanguliza Yanga kwa bao safi dakika ya 16 kupitia mpira wa adhabu kabla ya Jamus kusawazisha wakitumia makosa ya chipukizi kutoka U20 Mtita aliyechelewa kuondoa mpira katika eneo la hatari
Kipindi cha pili Jamus Fc walipaki basi huku wakitumia mashambulizi ya kushitukiza
Kocha wa Yanga Miguel Gamondi alilazimika kuwaingiza Max Nzengeli na Skudu ambao kwa kiasi kikubwa waliongeza kasi ya mashambulizi ya Yanga
Ni ushindi ambao unaendelea kuiweka Yanga kileleni mwa kundi C baada ya kufikisha alama sita na mabao saba ya kufunga ikiruhusu bao moja
Kimahesabu tayari Yanga imetinga robo fainali ya michuano hiyo


