Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewatoa hofu Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo juu ya alipo kinara wa mabao ligi kuu ya NBC msimu huu, Stephane Aziz Ki
Kamwe amesema Aziz Ki tayari amewasili jijini Dar es salaam na atakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri mkoani Mbeya kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu unaofuata Jumapili
"Kumekuwa na maswali mengi kuhusu Stephane Aziz Ki, niwaaambie tu, Aziz Ki tayari ametua jijini Dar es salaam na tutarajie atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo unaofuata"
"Pia tunategemea mlinda lango Djigui Diarra atawasili wakati wowote baada ya kuwa amemaliza majukumu ya timu ya Taifa kule Ivory Coast," alisema Kamwe
Katika mechi nne zilizopita, Yanga imewakosa idadi kubwa ya nyota wake waliokuwa katika majukumu ya timu za Taifa kutokana na michuano ya Afcon 2023 ambayo itafikia tamati huko Ivory Coast Jumapili
Habari njema kwa Wananchi ni kuwa wachezaji wote wanaweza kupatikana kuanzia mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa uwanja wa Sokoine, Jumapili