Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya CR Belouizdad ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano wa maandalizi ya mechi, Gamondi amesema anatambua mchezo huo utakuwa mgumu lakini ni matokeo ya ushindi pekee ambayo yataweka hai matumaini ya Yanga kusonga mbele hatua inayofuata
"Ni mchezo mkubwa na wa aina yake, lakini kwetu sisi ni mchezo ambao tunatakiwa kushinda kwa namna yoyote ile ili tuweze kusonga mbele. Tumefanya maandalizi mazuri na akili yetu yote inaangalia mchezo wa kesho"
Gamondi ameongeza kuwa itakuwa mechi yenye ushindani wa kimbinu lakini Yanga imejiandaa vyema akiamini kila mchezaji atatimiza majukumu yake kutekeleza kile ambacho wamekiandaa
"Tunatarajia utakuwa mchezo wenye mbinu nyingi hasa wakati gani wa kushambulia na wakati gani wa kujilinda na tumeyafanyia kazi maeneno yote mawili na kuhakikisha tutatumia vizuri kila nafasi tutakayoipata kwenye mchezo wa kesho," alisema
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, beki Dickson Job amesema wachezaji wamejipanga na watapambana katika mchezo huo ili kupata ushindi ambao utawaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele hatua inayofuata
"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tumejiandaa vizuri na mchezo wa kesho, mwanzo lengo lilikuwa ni kuingia hatua ya makundi baada ya muda mrefu lakini sasa lengo letu kwa pamoja ni kupambana na kusonga mbele zaidi kwa kila mchezo uliokuwa mbele yetu," alisema