Katika kila mechi ya nyumbani kwenye michuano ya ligi ya mabingwa, Yanga imejiwekea utaratibu wa hamasa ya mechi kupewa mchezaji
Alianza Maxi Nzengeli akafuata Stephane Aziz Ki, Ibrahim Bacca na Pacome Zouzoua huku mechi moja akipewa heshima hiyo GSM
Wakati akizungumza na wanahabari jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe alisema utaratibu huo utaendelea katika mchezo wa mkondo wa kwanza robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaopigwa Jumamosi ya March 30 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Hata hivyo Kamwe hakumtaja mchezaji huo akibainisha kuwa jina lake litawekwa hadharani wiki ijayo pale watakapozindua kampeni ya hamasa kuelekea mchezo huo
Miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kupewa heshima hiyo ni Khalid Aucho, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Yao Kouassi na mlinda lango Djigui Diarra


Aucho ameendelea kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti kuna nafasi kubwa atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Mamelodi
Bado kuna hatihati upande wa Yao kwani alichanika nyama za paja katika mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc sasa akiendelea na matibabu huku uongozi ukiweka bayana ana asilimia 50 za kucheza mchezo huo

Musonda, Diarra na Mudathir wao wako fit wakiwa katika majukumu ya timu za Taifa
Pengine uongozi wa Yanga umeweka kiporo ili wachezaji wote warejee kikosini, wiki ijayo wataweza kubaini wale ambao watakuwepo katika mchezo husika kwani utaratibu waliojiwekea Wananchi ni kuwa mchezaji anayepewa hamasa ya mechi lazima awe sehemu ya kikosi siku ya mechi husika