Jana baada ya mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns kocha wa timu hiyo Rulani Mokoena alionekana akijaribu kumnong'oneza jambo Stephane Aziz Ki ambaye alikuwa na huzuni baada ya kuishuhudia Yanga ikiondoshwa kwa mikwaju ya penati hatua ya robo fainali CAF CL
Alikuwa Kocha Msaidizi Moussa Ndaw aliyemuondoa Mokoena mikononi mwa Aziz Ki huku picha za video zikimuonyesha Ndaw akionekana kukerwa na kitendo kilichofanywa na kocha huyo
Mokoena lifanya tukio kama hilo baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na kimsingi alikuwa akijaribu kumshawishi Aziz Ki kujiunga na Sundowns
Ukipita katika kurasa za mashabiki wa Sundowns mijadala yao ni kuhusu Aziz Ki wakiwataka viongozi wao wahakikishe wanamsajili
Aziz Ki ameweka msimamo wake wazi kuwa hana mpango wa kuondoka Yanga kwa sababu bado hajakamilisha kazi iliyomleta Tanzania
Baada ya kuandika ujumbe wa shukrani kwa kuhitimisha safari yao ya ligi ya mabingwa msimu huu, baadhi ya mashabiki walikuwa na shauku ya kufahamu hatma yake kama ataendelea kubaki au anaondoka?
"Sina matarajio ya kuondoka Yanga kwa sasa kwani sijafanikisha malengo yaliyonileta hapa, bado klabu hii ninayoipenda kwa moyo wangu wote inanidai, hata pesa haitaweza kujaza upendo nilionao kwa klabu hii, lala kwa amani shabiki bado sijamaliza dhamira yangu," Aziz Ki alimjibu mmoja wa mashabiki