Mabingwa watetezi wa michuano ya kombe la FA (CRDB Bank Federation Cup) Yanga leo majira ya saa 2:30 usiku watakuwa uwanja wa Azam Complex kumenyana na Tabora United katika mchezo wa robo fainali
Yanga imepania kutetea taji hilo kwa msimu wa tatu, dakika 90 za mchezo dhidi ya Tabora United zinaweza kuwasogeza karibu katika kutimiza mpango wao kwani matokeo ya ushindi yatawapeleka nusu fainali
Utakuwa mchezo wa pili kuzikutanisha Tabora United na Yanga msimu huu. Timu hizo zilichuana katika mechi ya ligi kuu duru ya kwanza, Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma
Bado timu hizo zitakutana tena katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa hapo hapo Azam Complex ambako leo unapigwa mchezo wa FA
Baada ya kukosekana uwanjani kwa takribani wiki tano, mashabiki wa Yanga leo wanaweza kumshuhudia kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua akirejea baada ya kupona majeraha
Katika Mkutano na Waandishi wa Habari jana, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi alisema nyota huyo amepona na pengine anaweza kumpatia dakika chache katika mchezo huo kutegemeana na utimamu wake baada ya mazoezi ya mwisho
Msimu huu Yanga imekuwa na rekodi nzuri katika dimba la Azam Complex ikishinda mechi zote ilizocheza katika uwanja huo
Matarajio ya Wananchi ni kuona timu yao ikiendeleza ubabe na kutinga nusu fainali ya kombe la FA kwa ushindi dhidi ya Tabora United