Jana nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto alitoa 'assist' ya bao la tatu lililofungwa na Clement Mzize na kuwahakikishia Wananchi ubingwa wa tatu mfululizo ligi kuu ya NBC
Ni ubingwa wa 30 kwa Yanga katika historia ya Ligi Kuu. Akiwa nahodha hili linakuwa taji la tatu kunyanyuliwa nae tangu aliposajiliwa na Yanga akitokea klabu ya Coastal Union misimu minne iliyopita
Kumekuwa tetesi nyingi kumuhusu beki huyo tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuhusu hatma yake na Yanga
Mwamnyeto amewahakikishia Wananchi bado yupo sana hadi pale uongozi wa Yanga utakapomwambia imetosha
Akizungumzia ubingwa ambao Yanga walitwaa kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1, Mwamnyeto alisema ubingwa huo wameutoa zawadi kwa mashabiki wote ambao wamekuwa bega kwa bega na timu yao
"Ubingwa huu sio wa wachezaji au viongozi, huu ni ubingwa wa mashabiki wetu ambao wamekuwa nasi wakituunga mkono katika kila mechi mpaka kufikia siku ya leo," alisema Mwamnyeto
Mwamnyeto amekuwa nahodha wa Yanga kwa misimu minne ambapo amenyanyua takribani mataji saba, taji la ligi kuu msimu huu litakuwa na nane
Yanga bado haijamaliza kuvuna mataji msimu huu, kwani katika michuano ya kombe la FA iko hatua ya nusu fainali na itacheza na Ihefu Fc May 19 mchezo wa hatua hiyo utakaopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha