Tukio alilofanya kiungo wa Azam Fc Feisal Salum kutumia ishara ya kuwanyamazisha mashabiki baada ya kufunga mkwaju wa penati ni mwendelezo wa mchezaji huyo kutengeneza uhasama dhidi ya timu ambayo unaweza kusema ndio iliyompa jina
Kazi za shabiki wa mpira wa miguu ni mbili tu, kuzomea na kushangilia, lakini kazi ya mchezaji ni moja tu, kucheza mpira
Njia pekee ya kuwanyamazisha mashabiki ni kuiacha miguu yako izungumze lakini kutengeneza 'bifu' na kutaka kujibizana na mashabiki haiwezi kumsaidia mchezaji
Tukio alilofanya Feisal kama ingekuwa mechi ya ligi kuu angeadhibiwa maana, ishara hiyo aliyotumia hairuhusiwi kwani inaweza kuchochea vurugu kutoka kwa mashabiki
Lakini pia alichofanya Feisal ni kama alitukana mamba wakati bado hajavuka mto, kwani licha ya Yanga kuanza mikwaju ya penati kwa kusuasua ilifanikiwa kutetea taji la FA kwa msimu wa tatu mfululizo
Baada ya ushindi wa Yanga, Feisal hakuonekana tena uwanjani ikiwa ni pamoja na kukacha medali yake ya ushindi wa pili