Yanga iko sokoni kusaka winga wa kuchukua nafasi ya Augustine Okrah ambaye taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga imethibitisha Mghana huyo mkataba wake umesitishwa bada ya makubaliano ya pande mbili
Okrah alitua Yanga mwezi Januari katika dirisha dogo la usajili lakini ameshindwa kumshawishi Kocha Miguel Gamondi ambaye amehitaji kuletewa 'mtu mwingine' katika nafasi yake
Okrah anakuwa mchezaji wa pili kutoka Ghana kushindwa 'kutoboa' katika kikosi cha Yanga msimu huu baada ya Hafiz Konkoni
Konkoni alitua Yanga katika dirisha kubwa la usajili la msimu uliopita lakini miezi sita ilitosha kwa Yanga kumpa mkono wa kwaheri akitolewa kwa mkopo huko Libya
Linapokuja suala la maamuzi pale mchezaji ameshindwa kufikia mahitaji ya klabu, Yanga haijawahi kuwa na kigugumizi katika kuchukua hatua
Zipo gharama ambazo Yanga inalazimika kulipa katika kumalizana na wachezaji hao lakini pengine utaratibu huo ndio umepelekea wachezaji kupambania nafasi zao kwani wanafahamu kama watacheza chini ya kiwango 'Thank You' zitawahusu