Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amebainisha kuwa malengo ya klabu hiyo msimu ujao ni kufanya vizuri zaidi hasa katika michuano ya ligi ya mabingwa hivyo watafanya usajili 'mkubwa'
Kumekuwa hofu miongoni mwa Wananchi baada ya taarifa ya TFF juu ya kufungiwa kwa Yanga kutokana na madai ya wachezaji waliowahi kuitumikia timu hiyo
Juzi Kamwe alitoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo ambapo amethibitisha Yanga ilishamalizana na wachezaji hao na kinachosubiriwa ni uthibitisho kutoka kwa wahusika ili waweze kufunguliwa kusajili
"Jambo hili limemalizika kama nilivyozungumza mwanzo, tutafanya usajili na nawaambia tu, wajipange msimu ujao kwani tabu iko palepale," alisema Kamwe
Aidha Kamwe ametamba kuwa yule mchezaji maalum ambaye bango lake litawekwa pale Kariakoo atatambulishwa katika wiki ya Mwananchi huku timu hiyo ikitarajiwa kuanza kutangaza usajili wake kuanzia Julai 1
"Kuanzia Julai 1 tutaanza kutoa taarifa za usajili wetu. Tutatoa taarifa za wachezaji tuliachana nao, walioongeza mikataba na wale wapya tuliowasajili," aliongeza Kamwe