Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii amewapa nafasi mashabiki wa Yanga kupendekeza timu ambayo wangependa ialikwe katika kilele cha wiki ya Mwananchi August 04
Maoni ya wengi yameangukia kwa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Pengine ni kutokana na kile kilichotokea katika robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa msimu uliopita Yanga ikiondoshwa kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana kwa dakika 180
Lakini Wananchi wanaamini walistahili kutinga nusu fainali kwa sababu timu yao ilifunga bao halali kupitia Stephane Aziz Ki lakini waamuzi wakalikataa
Rais CAF Patrice Motsepe alipokuja nchini kushuhudia michuano ya CAF kwa shule za Sekondari ambayo ilifanyika Zanzibar mapema mwaka huu, alikiri kuwa Yanga ilionewa kwa bao lao kukataliwa katika mchezo huo wa mkondo wa pili uliopigwa Afrika Kusini
Maneno haya ilikuwa kama kuwapoza Wananchi tu kwani Motsepe ndio mmiliki wa Sundowns na maamuzi hayo mabovu yaliinufaisha timu yake kwani baada ya kutinga nusu fainali walijihakikishia kushiriki michuano ya kombe la Dunia ya klabu itakayofanyika 2025 nchini Marekani. Michuano hiyo itashirikisha timu 32 na itaendeshwa na FIFA kwa utaratibu sawa na ule wa kombe la Dunia
Sasa Wananchi wanawataka Sundowns ili wamalizane mapemaaa kabla ya kukutana katika mashindano maalum
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga imebainisha kuwa Sundowns ni miongoni mwa ambazo Yanga inalenga kuzialika
Hata hivyo upatikanaji wa timu hiyo inaweza kuwa changamoto kwani nao wana ratiba yao ya pre-season ambayo inafanyika barani Ulaya
Julai 28 Yanga itakuwa Afrika Kusini kuchuana na Kaizer Chiefs katika mchezo wa Toyota Cup ambapo baada ya mchezo huo watarejea nchini tayari kwa kilele cha wiki ya Mwananchi