Leo bingwa mpya wa Ngao ya Jamii atafahamika pale Yanga itakaposhuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuchuana na Azam Fc katika mchezo utakaopigwa saa 1 usiku
Hii ni fainali nyingine kuzikutanisha Yanga na Azam Fc baada ya timu hizo kukutana katika fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita na Yanga kubeba taji
Unaweza kusema kwa sasa Azam Fc ndiye mpinzani wa kweli wa Yanga katika soka la ndani kwani timu hiyo imekuwa ikitoa upinzani mkali katika mechi wanazokutana na Yanga
Mechi ya leo haitakuwa tofauti na mechi zilizopita lakini baada ya dakika 90 mshindi atapatikana na kama sivyo mikwaju ya penati itatumika
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ametamba kuwa kikosi chake kiko tayari na yeye binafsi anapenda kucheza mechi ngumu
Kabla ya mtanange huo, mapema saa 9 utachezwa mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Simba dhidi ya Coastal Union
Simba ilitupwa nje ya mashindano kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga wakati Coastal Union wakipoteza kwa kufungwa mabao 5-2 na Azam Fc