Yanga imeanza vyema michuano ya ligi ya mabingwa 2024/25 ikipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Vital'o ya Burundi
Prince Dube ameendeleza kasi yake ya kupachika mabao akiwa na uzi wa Yanga akifunga bao la uongozi mapema tu katika dakika 6
Ni kama Vital'o walikuwa na matumaini baada ya kwenda mapumziko wakiwa wameruhusu bao moja lakini walikumbana na Yanga yenye sura tofauti katika kipindi cha pili hasa baada ya Gamondi kuwaingiza Pacome Zouzoua, Clement Mzize na Kennedy Musonda
Clatous Chama ndiye aliyefunga bao la pili akimalizia shuti la Aziz Ki lililogonga mwamba kabla ya Clement Mzize kufunga bao la tatu dakika chache baadae akitumia makosa ya mlinzi wa Vital'o kurejesha pasi fupi nyuma
Alikuwa Stephane Aziz Ki aliyefunga bao la nne katika dakika za majeruhi kwa mkwaju wa penati baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari
Ni ushindi ambao umeiweka Yanga katika hatua nzuri ya kutinga raundi ya kwanza kwani katika mechi ya marudiano itahitaji sare tu
Mechi ya pili itapigwa August 24 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga wakiwa wenyeji