Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' keshokutwa Jumatano, Septemba 04 itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kumenyana na Ethiopia katika mchezo wa kwanza kundi H kuwania tiketi ya kufuzu Afcon 2025
Tanzania, Ethiopia, DR Congo na Guinea ziko katika kundi H ambapo timu mbili zitakazomaliza nafasi za juu zitajihakikishia tiketi ya michuano hiyo itakayofanyika Morocco
Mkakati wa Stars ni kuhakikisha inafuzu kwa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushiriki michuano iliyopita iliyofanyika Ivory Coast mapema mwaka huu
Tanzania, Kenya na Uganda zitaandaa kwa pamoja Afcon 2027, hivyo kila nchi imepewa mkakati wa kuhakikisha inafuzu kwa Afcon 2025 na kutumia michuano hiyo kujiongezea uzoefu
Kikosi cha Stars kimekamilika baada ya wachezaji wa Yanga kujiunga na timu. Nyota hao walijiunga na kikosi baada ya kukamilisha mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar ambao Wananchi walishinda mabao 2-0