Klabu ya Yanga imekuja na mkakati kabambe wa kuhakikisha inakwenda kukamata nafasi ya kwanza kwenye Ligi Kuu kuanzia kesho itakapocheza dhidi ya Pamba Jiji, Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa mabingwa hao wa nchi, Ali Kamwe, amesema kuwa pamoja na kushinda michezo yao mitatu, lakini bado hawatokuwa na furaha hadi hapo watakapohakikisha wamekamata nafasi ya kwanza ambayo ndiyo sehemu waliyoizoea
"Operesheni hii ni kuisaka namba moja, tutaianza rasmi Alhamisi tutakapocheza dhidi ya Pamba Jiji, niseme tu kuwa tuko katika harakati ya kuisaka nafasi ya kukaa kileleni"
"Tumekusanya pointi tisa, tuko vizuri kidogo katika msimamo wa Ligi Kuu, ila nafasi yetu pendwa ni namba moja, tutaanza rasmi kuisaka kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji, tunaelekea kileleni na hakuna wa kutuzuia," alisema Kamwe
Kamwe amewataka mashabiki kuwa sambamba na timu kwani jambo hilo halitokuwa rahisi kama wao watakaa majumbani, inabidi wajazane uwanjani kwa ajili ya kuwaunga mkono viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji
"Timu ambazo hazijaanza vyema zikicheza na Yanga zinakamia sana, tuliona mchezo na KenGold, tukashuhudia dhidi ya KMC, kwa hiyo hata Pamba Jiji haitokuwa rahisi, kwa hiyo mashabiki wanatakiwa wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuungana katika mkakati wa kuelekea kwenye nafasi ya kwanza," alisema