Mechi yake ya kwanza dhidi ya Simba msimu uliopita ulikuwa mchezo wa fainali Ngao ya Jamii ambao ulimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana na baadae Simba kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 4-3 katika mchezo ambao wengi wanaamini kama isingekuwa makosa ya kibinadamu ya waamuzi pengine mambo yangekuwa tofauti
Baada ya mchezo huo makala nyingi zikaandikwa kumsifu Kocha wa Simba wakati huo Robertinho Oliveira kuwa ni kiboko ya Yanga kwani hajawahi kupoteza mchezo dhdi ya Yanga katika timu zote alizofundisha
Ikumbukwe Yanga ilikuwa imetoka kupoteza kwa mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu msimu mmoja nyuma wakati huo ikinolewa na kocha Nasreddine Nabi
Gamondi akaziandaa silaha zake, kwa hakika Novemba 07 2023 ikawa siku ya kukumbuka kwake akiishushia Simba kipigo cha mabao 5-1 pale Lupaso
Ni kipigo kilichoondoka na ajira ya Robertinho ambaye licha ya kuwa mchezo wake wa kwanza kupoteza, hakukuwa na uvumilivu tena kwa viongozi wa Simba
Mchezo wa pili dhidi ya Simba msimu uliopita akakutana na kocha raia wa Algeria Abdelhak Benchikha ambaye aliajiriwa na Simba kuchukua nafasi ya Robertinho aliyetimuliwa baada ya kipigo cha Novemba 07
Ni kipigo cha mabao 2-1 ambacho Simba walikipokea kwa mara ya pili mfululizo kilichochea kuondoka kwa Benchikha
Kwani baada ya kipigo hicho, Benchikha alishusha lawama kwa wachezaji wake kuwa ni wagumu kuelewa, siku chache baadae akatangaza kuachia ngazi
Fadlu Davids ni kocha wa tatu kukutana na Gamondi na tayari ameshapokea kichapo mara moja ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii, Yanga ikishinda bao 1-0 mechi ya nusu fainali iliyopigwa August 08
Oktoba 19 Fadlu raia wa Afrika Kusini anakutana tena na Gamondi katika mechi ambayo kama atajichanganya tena kama watangulizi wake, 'atasema'
Wenzie wawili waliachia siti muda mfupi baada ya kukutana na kipigo cha Gamondi, Jumamosi inaweza kuwa zamu yake kupisha siti kwa mwingine...!