Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema watakuwa tayari kuikabili Coastal Union hapo kesho katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid lakini hilo haliondoi ukweli wanakabiliwa na ratiba ngumu
Baada ya kalenda ya mechi za Kimataifa kuwania kufuzu fainali za Afcon 2025 kuhitimishwa Oktoba 15, mchezo wa dabi ya Kariakoo ulipigwa Oktoba 19 Yanga ikiathirika zaidi kwani ilikuwa na wachezaji 12 katika timu za Taifa
Oktoba 22 Yanga ikashuka uwanja wa Azam Complex kuikabili JKT Tanzania na jana timu ikasafiri Arusha kwa ajili ya kuikabili Coastal Union hapo kesho Oktoba 26
Baada ya mchezo huo Yanga itasafiri visiwani Zanzibar kuikabili Singida Black Stars Oktoba 30
Gamondi amesema hawapaswi kulalamika zaidi ya kupambana na ratiba hiyo lakini ni kweli haitoi muda wa kupumzika kwa wachezaji
"Kwanza nimefurahi sana kuwa Arusha tena, kiukweli tuna ratiba ngumu kidogo, tumejaribu kupangilia ratiba yetu tupate angalau muda wa kupumzika"
"Hatupaswi kulalamika isipokuwa kupambana na hali halisi, ingawa ukweli ni kwamba hii sio ratiba nzuri ya kujiandaa na mchezo"
"Yanga tuna utajiri mkubwa wa vipaji ambao unanipa wasaa wa kutumia mfumo wowote bila kuathiri ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja"
"Ingawa mimi siamini sana kwenye mfumo bali namna gani sahihi ya kutengeneza nafasi na kuzitumia. Nina mawasiliano mazuri sana na wachezaji wangu wote licha ya kwamba sio wote wanapata nafasi," alisema