Nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto amesema malengo yao kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Singida Black Stars hapo kesho ni ushindi
Yanga inaelekea Zanzibar kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa uwanja wa New Amaan Complex, Jumatano saa 2:30 usiku
Mwamnyeto amewataka mashabiki wa Yanga visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo kuwaunga mkono
"Mechi itakuwa ngumu, Singida ni timu nzuri na imesajili wachezaji wazuri sana msimu huu, lakini kwetu Yanga msimamo wetu ni ule ule, kukusanya pointi tatu kila mchezo"
"Tutapambana ili kuendeleza kile tulichofanya katika mechi zilizopita, tunachohitaji kila mchezo ni pointi tatu," alisema Mwamnyeto
Nae Nahodha Msaidizi Dickson Job, amesema wataendelea kucheza pamoja kama timu ili kuhakikisha hawaruhusu bao katika mchezo huo kama walivyofanya kwenye mechi zilizopita
Job amefichua mbinu za kocha Miguel Gamondi kuzuia pamoja wanapokuwa hawana mpira, zimechangia kuwafanya wasiruhusu bao msimu huu
"Huwa tunacheza kwa mifumo mingi, lakini mara nyingi tunasaidiana majukumu, tunapokwenda kushambulia tunawasaidia kidogo, lakini tunaposhambuliwa siyo jukumu la mabeki peke yake, kukaba linakuwa ni jukumu la wachezaji wote kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji"
"Mfumo huu umekuwa ukitufanya mabeki tuwe na ufanisi kwenye kazi yetu," alisema Job