'The Wonderkid' Denis Nkane jana alifanya maajabu yake katika mchezo wa ligi kuu ya NBC dhidi ya Singida Black Stars akitumika nafasi ya ulinzi upande wa kulia katika mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Mara kadhaa Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi alieleza sababu ya kumtumia Nkane kama beki badala ya winga akiamini kijana anaweza kucheza vyema nafasi hiyo
Katika mechi yenye presha kubwa, hakuna aliyetarajia kama Nkane atamudu mikiki mikiki ya mchezo huo hasa ikizingatiwa ametumika eneo ambalo ni kama majaribio
Lakini dakika 90 za mchezo dhidi ya Singida BS zimedhihirisha Nkane sasa anaweza kutimiza majukumu ya safu ya ulinzi upande wa kulia pale Yao Kouassi anapokosekana
Na pengine sio hivyo tu, Gamondi anaweza kumtumia Nkane katika nafasi hiyo bila ya kujali uwepo wa Yao
Hii sio habari nzuri sana kwa Kibwana Shomari ambaye ameongezewa ushindani katika nafasi yake lakini ni habari nzuri kwa Gamondi ambaye kikosi chake kinazidi kuwa imara