Kabla ya mchezo dhidi ya Simba Oktoba 19, takribani wachezaji 12 wa Yanga walikuwa katika majukumu ya timu za Taifa
Baadhi ya wachezaji walichelewa kurejea kutokana na changamoto ya usafiri akiwemo mlinda lango Djigui Diarra ambaye alitua nchini saa 3 kabla ya mchezo
Hata hivyo wachezaji wa Yanga walipambana na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ambayo ilikuwa na asilimia 95 kikosi chake
Oktoba 22 Yanga ikashuka tena dimbani kucheza na JKT Tanzania na kushinda mabao 2-0
Baada ya mchezo huo Yanga ikasafiri mkoani Arusha kuikabili Coastal Union katika mchezo uliopigwa dimba la Sheikh Amri Abeid Oktoba 26 na kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Walivyotoka Arusha Wananchi wakaelekea Zanzibar kuikabili Singida Black Stars Oktoba 30 katika mchezo mgumu ambao Wananchi walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Jana Yanga ikashuka tena uwanja wa Azam Complex siku tatu baada ya kuikabili Singida BS
Mechi ya mwisho kwa Azam Fc ilikuwa dhidi ya KenGold Oktoba 25 hivyo wao walipata wiki nzima ya kupumzika kabla ya kucheza na Yanga huku Wananchi wakicheza mechi mbili ngumu katika siku saba kabla ya mechi yao na Azam Fc
Ni wazi ilikuwa ratiba ngumu kwa Yanga, na zaidi katika mchezo dhidi ya Azam Fc mapema tu wakapoteza mchezaji muhimu na kulazimika kucheza zaidi ya dakika 70 wakiwa pungufu
Wachezaji wa Yanga na benchi la ufundi wanastahili pongezi kwa kupambana katika ratiba hiyo na kufanikiwa kuchukua alama 12 kati ya alama 15
Katika kipindi cha siku 14 Yanga imecheza dhidi ya Simba, JKT Tanzania, Coastal Union, Singida Black Stars na Azam Fc katika mechi zilizopishana siku tatu hadi nne!